BAADA ya staa wa muziki wa Bongo Fleva na muuza sura katika video mbalimbali za wasanii wa muziki ambaye kwa sasa ni mjamzito, Gift Stanford ‘Gigy Money’ kukiri hivi karibuni kwamba anapigwa na mpenzi wake anayejulikana kwa jina la Moj, imeelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kichanga chake kufia tumboni.
Awali, Gigy Money aliandika waraka mzito kupitia page yake ya Instagram akielezea mateso anayoyapitia kwenye mapenzi kwa sasa huku akisema anachukia mwanaume anayepiga wanawake wajawazito.
“Kiukweli leo nina stress sana na ndiyo maana nimeona bora niseme kwani ninachokiamini mimi siyo peke yangu ninayeyapitia haya kuna muda unaweza ukakufuru Mungu kwa maneno ambayo kesho na keshokutwa huwezi kuyarudisha kinywani, katika makosa ambayo najua nimeyafanya ni kupenda lakini kupenda siyo dhambi, nimepitia mengi sana kwenye mapenzi kiasi cha kufikia kupungua kimwili.
“Hakuna kitu kibaya na kigumu kama kumuaminisha mtu unampenda, unaweka nguvu na jitihada zako katika mapenzi kuna muda unawaza sijui niachie ngazi kwani unayempenda yawezekana anampenda mtu mwingine na anayekupenda humpendi hata kidogo… nimepitia vingi sana kwa watu walio karibu nami wanaweza wakawa wanajua baadhi ya mateso na utumwa wa mapenzi niliowahi kupitia na bado najiuliza kwa nini wanaume ni wagumu kuonesha hisia zao za ukweli? Inashangaza mwanaume anaweza kuishi na wewe pika pakua lakini anayempenda yuko mbali na upeo wa macho yake.
“Wanaume wa Bongo wajeuri, unabeba mimba dharau atakufanyia mwanamke wake wa nje atakuonesha, kiukweli inauma ndiyo lakini naamini ni hatua za maisha na ukuaji, naamini nimedondoka hatua moja lakini naweza kuinuka hatua 8, Tanzania ni nchi inayoongoza kuwa na single mother’s siyo, wote baba wa watoto wamefariki wengi wetu huwaga tunawakimbiza watoto wetu mbali na maisha na mateso tuliyowahi kuyapitia kwa baba zao, hakuna mtu anayeweza kunielewa ila mkiona mtu anaandika hivi ujue yanazidi…,” ilisomeka sehemu ya waraka huo.
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Gigy ili kueleza zaidi kuhusu mateso aliyokiri kwamba anayapitia kwenye waraka huo lakini simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu chochote.
Kutokana na Gigy kueleza mateso hayo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta daktari anayejulikana kwa jina la Marise Richard wa Marise Dispensary na kueleza kuwa, kama staa huyo anapigwa na kupewa stresi nyingi, kuna hatari kubwa ya kichanga kilicho tumboni mwake kufa.
“Kumpiga mwanamke mjamzito ni hatari sana kwani mimba inaweza kuharibika na kama kiumbe kimeshakuwa cha miezi kadhaa kinaweza kufa tumboni, hivyo vipigo kwa wanawake wajawazito ni hatari,” alisema Dokta Marise.
MSIKILIZE MPENZI WAKE
Ili kuujua ukweli wa waraka huo wa Gigy, gazeti hili lilimtafuta Moj na kumuuliza kuhusiana na madai hayo ya kumpiga Gigy ambapo alisema hayana ukweli.
“Unajua mwanamke siku zote akiwa mjamzito anakuwa na hasira sana na ndiyo inayotokea kwa Gigy, wakati mwingine anakuwa na hasira kupitiliza ndiyo anaandika mambo ya ajabu kama hayo, simpigi na hakuna kitu kama hicho kabisa,” alisema Moj
No comments:
Post a Comment